Wakazi wa wadi ya Birongo, eneo bunge la Nyaribari chache kaunti ya Kisii wameandamana kulalamikia barabara mbovu katika wadi hiyo ambazo hazipitiki msimu huu wa mvua.
Wakazi hao waliandamana siku ya Jumanne na kuchimba barabara hizo huku wakipanda migomba ya ndizi wakidai ni shamba.
Wakizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumaane katika eneo la Keroke, Victor Onkoba, aliyezungumza kwa niaba ya waandamanaji hao alisema wamekuwa wakidanganywa kukarabatiwa barabara hizo kwa muda mrefu sasa, na hakuna chochote kimefanyika na kuwalazimu kuandamana kumlazimu mwakilishi wa wadi hiyo Geofrey Nyamache kukarabati barabara za wadi yake.
Baadhi ya barabara wakazi hao wanahitaji zikarabatiwe ni miongoni mwa barabara ya kutoka Birongo-Keroke-Taraacha, Birongo–Irondi na zingine ambazo hazipitiki kamwe.
“Tangu mvua ianze kunyesha hapa Kisii, barabara hizi hazipitiki, tumeshindwa la kufanya na mwakilishi wetu Geoffrey Nyamache amekuwa akitudanganya kuwa atakarabati barabara hizi lakini hajawahi tukarabatia,” alisema Onkoba mwandamanaji pia mkazi wa Birongo.
"Hii leo tumeandanana na tutaendelea kuandanmana hadi tukarabatiwe barabara hizi zetu ili wafanyibiashara na wakulima kupata mahala pa kupita," aliongezea.