Wakazi wa wadi ya Esise, eneo bunge la Borabu Kaunti ya Nyamira wamelalamikia ongezeko la wizi wa ng’ombe kila wakati na haswa nyakati za usiku.
Kulingana na wakazi hao, wamekuwa wakipata hasara kubwa kufuatia wizi wa mifugo wao, huku wakidai kuwa maafisa wa polisi hawashirikiani nao kupunguza wizi huo baada ya kupiga ripoti kwao kila wakati.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne katika kijiji cha Riamogambi, wakazi hao, wakiongozwa na Joseph Orina, waliomba maafisa wa polisi kutoa usaidizi kwao kwa kuwapunguzia wizi huo kwani wamekuwa wakipata hasara si haba.
Wakati huo huo, wakazi hao walisema wiki jana zaidi ya ng’ombe watatu waliibwa na kuvushwa mpaka wa Kipsigis, huku wakiomba usaidizi kutoka kwa polisi ili kudhibiti visa hivyo.
“Tunaomba maafisa wa polisi kuwasaka na kuwatia mbaroni wezi ambao wanaendelea kutuibia mifugo wetu kutoka zizi zetu hapa,” alisemaOrina.
Aidha, wakazi hao waliomba serikali kujenga kituo cha polisi katika mpaka huo ili kukabiliana na wezi wanapovuka mpaka huo.
“Tunaomba kituo cha polisi kijengwe kwa mpaka wa Kisii na Kipsigs ili wezi wakabiliwe vilivyo,” aliongezea Orina.