Wakazi wa eneo la uwakilishi wodi ya Gesima wamejitokeza kuipongeza serikali ya kaunti ya Nyamira kwa hatua iliyochukua serikali hiyo kuhakikisha kwamba hospitali ndogo ya Mochenwa imepanuliwa.
Wakihutubu wakati wa ufunguzi rasmi wa mradi huo siku ya Jumapili, wakazi hao walisema hatua hiyo itawasaidia watu wengi kupata huduma za hospitali.
"Ningependa kuishkuru serikali ya kaunti hii kwa hatua yake ya kuharakisha upanuzi wa hospitali hii kwa maana sasa jengo hili jipya litahifadhi idadi kubwa ya wagonjwa, na hiyo itakuwa njia mojawapo ya kupunguza misongamano katika hospitali ya Nyansiongo kwa maana kuanzia sasa wagonjwa wengi watahudumiwa hapa," alisema Peterson Nyabwari.
Mwakilishi wa wadi ya Gesima Ken Atuti aliwasihi wakazi wa eneo hilo kuipa muda serikali ya kaunti hiyo ili ikamilishe baadhi ya miradi ambayo ingali kutamatika.
"Nikiwa mwakilishi wenu kwenye bunge la kaunti nimeweka mikakati ya kuhakikisha masuala ya barabara na miundomisingi, afya na kilimo yanaangaziwa na nina hakika serikali itayashughulikia na sharti tuipe muda," alisema Atuti.