Viongozi wa kisiasa kutoka kaunti ndogo ya Masaba wameombwa kuwahimiza wakazi wa eneo hilo kuhudhuria mikutano ya hadhara, hasaa mikutano ya bunge mashinani inayotarajiwa kufanyika katika eneo hilo hivi karibuni.
Akihutubu kwenye soko ya Rigoma siku ya Jumanne, mwakilishi wadi ya Rigoma Benson Sironga alisema kuwa wakazi wengi wamekuwa wakikwepa mikutano ya hadhara hasa ile inayoandaliwa na serikali ya kaunti ya Nyamira.
"Nawasihi viongozi wa kisiasa katika eneo hili hasa mbunge wa hapa kushirikiana na afisi yangu kuwahimiza wananchi kuhudhuria mikutano ya hadhara kwa kuwa mikutano hiyo hujadili maswala muhimu katika jamii," alisihi Sironga.
Mwakilishi huyo aidha aliongeza kwa kusema kuwa wakazi wengi wana mazoea ya kukwepa mikutano ya hadhara, huku akiwahimiza wakazi kuhudhuria mkutano wa bunge mashinani kwenye soko la Rigoma tarehe 12 mwezi huu kwa kuwa watapata fursa ya kuuliza maswali na pia kufahamu jinsi bunge la kaunti linavyoendesha shughuli zake.
"Wananchi wengi wana mazoea ya kukwepa mikutano ya hadhara, lakini nawaomba wakazi wa eneo hili kujitokeza kuhudhuria mkutano wa bunge mashinani kwenye soko la Rigoma kwa kuwa watapata nafasi ya kuuliza maswali nakujua jinsi bunge la kaunti ya Nyamira linavyoendesha shughuli zake," alisema Sironga.