Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa eneo la Kebirigo, Kaunti ya Nyamira, wameomba maafisa wa polisi kuwaimarishia usalama wao kwani wamekuwa wakishambuliwa na washukiwa wa ujambazi kila mara.

Hii ni baada ya mwanamume mmoja wa umri wa miaka 35 kutolewa kutoka kwa nyumba yake usiku wa kuamkia Jumatano na kuuawa.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano mjini Kebirigo, wakazi hao, wakiongozwa na mzee wa kijiji cha Kebagora Henry Kerunda, walisema wamehofia usalama wao kwani wamekuwa wakishambuliwa na watu wasiojulikana katika siku za hivi maajuzi.

“Tunaomba maafisa wa polisi kutuimarishia usalama wetu hapa Kebirigo kwa sababu mzee wetu ameuawa na watu wasijulikana,” alisema Kerunda.

Visa vya mashambulizi vimekuwa vikishuhudiwa kila mara katika kaunti ya Nyamira katika siku za hivi maajuzi, jambo ambalo limekosa suluhu mwafaka.

Ikumbukwe kuwa mapema mwezi wa Novemba, kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josephine Onunga alitangaza na kuwahakikishia wananchi wa kaunti hiyo kuwa usalama umeimarishwa katika kila sehemu, jambo ambalo bado halijazaa matunda.