Wakazi wa kijiji cha Kemera kwenye kaunti ndogo ya Manga wamelalamikia vikali hali mbaya ya barabara za maeneo hayo.
Wakiongozwa na mkazi mmoja Cyrus Ombongi, wananchi hao walilalamikia hali hiyo kwenye kituo cha kibiashara cha Kemera, ambapo waliiomba serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na serikali ya kaunti kutenga pesa zilizokuwa zimetengwa kwa minajili ya El-nino ili kukarabati daraja na barabara zilizoko katika hali mbaya.
"Tunaiomba serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na ile ya kaunti kutumia pesa zilizokuwa zimetengewa mvua ya Elnino ili kujenga madaraja ambayo yameanguka na pia kukarabati barabara katika eneo ili ili ituwie rahisi kusafirisha bidhaa na mazao ya shambani hadi sokoni," alisema Ombongi.
Ombongi aliongeza kwa kusema kuwa ikiwa hali hiyo haitarekebishwa, basi itawawia vigumu kusafirisha mazao na bidhaa zao sokoni kwa wakati unaofaa, huku akisisitiza kuwa hali hiyo itaadhiri sana maendeleo ya kaunti.
"Iwapo serikali haitarekebisha hali mbaya ya barabara na daraja katika sehemu hii, basi tutapata ugumu wa kusafirisha bidhaa na mazao yetu ya shambani kwenda sokoni kwa wakati unaofaa, na hiyo itaadhiri pakubwa maendeleo ya kaunti hii," aliongezea Ombongi.