Wakazi kutoka eneo la Tuff Gong, DC katika mtaa wa Kibera wamekadiria hasara baada ya moto kuzuka eneo hilo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Moto huo uliteketeza takriban vibanda 30 zikiwemo nyumba usiku Jumapili usiku.

Moto huo ulioanza saa tatu unusu usiku siku ya Jumapili na ulikisiwa kuanzishwa na mlipuko wa stima ambazo baadhi ya wakaazi wa maeneo hayo walisema kwamba moto huo ulianzia kwa mojawapo wa vyumba ambapo mwenyeji wa chumba hicho alikuwa anatumia stima aina ya tokens.

‘‘Tulisikia mlipuko kutoka kwa nyumba ya jirani mmoja na moto huo ukaanza na ulisambaa kwa kasi sana. Tulijaribu kukabiliana nao bali hatukufua dafu kwani hatukuwa na maji kwa karibu,’’ alisema mmoja wa waathiriwa wa moto huo.

Wakaazi hao aidha walilalamika juu ya ukosefu wa maji na miundo misingi mibovu ilichangia pakubwa kusambaa kwa moto huo uliosababisha hasara kubwa. Aidha, wazima moto kutoka kwa kaunti ya Nairobi na kundi kutoka kwa shirika la msalaba mwekundu walifika katika eneo la mkasa na kuuzima moto huo.

Baadhi ya waathiriwa wa mkasa huo aidha wameiomba kampuni ya umeme nchini, KPLC kutafuta mbinu rahisi ya kuzima stima kwa transformer haswaa wakati wa mikasa ya moto.

‘‘Tunaiomba kampuni ya KPLC iweke ofisi zake katika maeneo tofauti mtaani Kibera na iwasajili vijana watakaowajibika kwa kuzima transformer haswaa wakati wa mkasa wa moto,’’ alisema mwaathiriwa mwengine.

Kisa hiki cha moto katika maeneo ya DC kinajiri wiki mbili tu baada ya kisa kingine kujiri katika eneo la Olympic mtaani Kibera ambao ulisababishwa na kulipuka kwa mtungi wa gesi na ambapo zaidi ya vibanda vya biashara 10 viliteketea.