Wakazi wa eneo la Mbaruk, Kikopey na Kiundo wamo hatarini ya kupatwa na mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu pamoja na mengine yanayoletwa na uchafu, baada ya vyoo vingi kujaa maji ya mafuriko.
Mafuriko hayo ambayo wenyeji wanasema yanatoka nyanda za juu za milima ya Ngorika na Dundori tangia mvua ya Jumanne wiki hii yameadhiri wakazi wasiopungua 150, kwa kufurika hata kwenye nyumba zao, na kuua mifugo ikiwemo kuku.
Kulingana na mkazi mmoja Jonathan Mwangi, mfumo wa kuondoa maji ya mafuriko eneo hilo hauko sawa, na kwamba viongozi wa kaunti wameendelea kuwapuuza.
Naye Mary Mwangi, mkazi mwingine alihofia njaa itawapata kwani chakula kinaharibikia ghalani.
Hayo yakijiri, idadi ya waliolazimika kuhama makwao kutokana na mvua ya El-nino katika eneo la Solai imefikia 40.
Eneo hilo huadhirika pakubwa kiasi cha barabara ya Lower Solai kutokomea kwenye maji ya ziwa Solai hata wakati kuna mvua ya kadri.
Aidha, kulingana na chifu wa Ruiyobei Mark Mogotio, endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, basi maisha ya zaidi ya watu 500 yamo hatarini.