Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Bodi ya ardhi katika kaunti ya Kisii imewashauri wananchi kuwa macho na kutonunua shamba kabla ya kufanya uchunguzi wa kutosha.

Hii ni baada ya kubainika kuwa baadhi ya wamiliki wa mashamba mjini Kisii wanamiliki zaidi ya vyeti viwili vya ardhi kwa shamba moja na kuwauzia wanunuzi zaidi ya mmoja.

Hayo yalichipuka baada ya wanunuzi wawili wa shamba kuuziwa shamba moja katika eneo la Nyanchwa, kitongoji cha mjini Kisii, huku nambari za vyeti vya ardhi vikiwa tofauti lakini vinaashiria shamba moja.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano mjini Kisii, mwenyekiti wa bodi ya ardhi katika kaunti ya Kisii Ombasa Omweno alisema wanunuzi wa mashamaba wanastahili kufanya uchunguzi kabla ya kununua ardhi kwani watauziwa mara zaidi ya mbili na kupata hasara.

“Kuna baadhi ya wamiliki wa mashamba mjini Kisii wanamiliki shamba moja wakiwa na zaidi ya vyeti vitatu, na hayo tumethibithisha kutoka eneo la Nyachwa ambapo tayari wanunuzi wawili wameuziwa shamba moja huku kila mnunuzi akiwa na cheti cha ardhi hiyo,” alisema Omweno

Aidha, Omweno alikosoa baadhi ya maafisa wanaofanya kazi katika afisi hiyo ya ardhi ambao wanashirikiana na wamiliki wa mashamba kuwakabidhi vyeti zaidi ya kimoja kwa shamba moja, huku akiapa kuchunguza maneno hayo ili kuleta na kuonyesha ukweli kwa wananchi kutolaghahiwa.