Kufuatia wakazi wa eneo la Shika Adabu, Ujamaa, Kiwerera pamoja na Samaki Kaunti ya Mombasa kulalamikia kusumbuliwa na kunguni, waziri wa afya katika kaunti hiyo Binti Omar amewahakikishia kuwa atatuma maafisa wake kutathmini kero hilo la wadudu hao.
Amesema kuwa serikali ya kaunti ipo tayari kukabiliana si tu kero hilo, lakini kuhakikisha kuwa kila mkazi wa kaunti anapata huduma bora za afya na anaepushwa na maradhi ambayo yanaweza kuzuiliwa kupitia ushirikiano wa wizara yake na ile ya kitaifa.
Akiongea siku ya Jumatatu kwenye afisi ya kaunti hiyo ya Mombasa, Omar aliwataka wakazi kuwa na subira, huku akiahidi kuwapanga maafisa walio chini yake kuenda na kushughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo.
Hatua hiyo ya waziri huyo ni mojawapo ya harakati za kaunti kujaribu kushughulikia masuala yanayowaathiri moja kwa moja, na kufanya kazi kwa karibu na wakazi.
Itakumbukwa kuwa wakazi wa maeneo hayo matano kwa miezi mitatu sasa wamekuwa wakiumia kutokana na wadudu hao bila jirani kumwambia jirani mwenzake hadi wakati vyombo vya habari vilipofichua masahibu yao wiki jana, ndiposa wakazi walijitoa kimasomaso na kuelezea vile kunguni hao wamekuwa sugu kwenye dawa ambazo zinatumiwa dhidi yao.