Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi mjini Molo wameitaka serikali kuikarabati barabara ya Molo kuelekea, Kibunja huku wakisema kuharibika kwa barabara hiyo kunatatiza usafirishaji wa bidhaa pamoja na huduma mjini Molo.

Wakazi, haswa wafanyibiashara na wahudumu wa pikipiki wameitaka serikali kutimiza ahadi yake ya kuiweka lami barabara hiyo inayounganisha mji wa Molo na barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Wenyeji wamesema barabara hiyo imekuwa katika hali mbaya kwa zaidi ya miaka kumi, huku serikali kuu na ile ya jimbo la Nakuru zikitoa ahadi ambaoz hadi sasa haijatekelezwa.

“Shida ni moja tu, serikali itutengenezee barabara, vumbi na mashimo ni mengi katika barabara hii na inatusababishia madhara na uhalifu unashuhudiwa sana,” alisema mkazi mmoja.

Wamesema wahalifu wanatumia hali mbaya ya barabara hiyo kuteka nyara magari pamoja na pikipiki huku wananchi wakisema zaidi ya madereva watano wa bodaboda wemepokonywa pikipiki zao nyakati za usiku na wahalifu wasiojulikana wakiwa kwenye barabara hiyo.

Mwaka jana naibu wa rais William Ruto akiwahutubia wakazi wa molo katika shule moja wilayani humo alisema barabara hiyo itawekwa lami baada ya siku 60, lakini hadi sasa hakuna wanakadarasi wametumwa kufanya ukarabati.

Barabara ya Molo kuelekea kibunja pamoja na barabara ya Molo kuelekea Olenguruone ni baadhi ya barabara mbovu zaidi katika kaunti ya Nakuru, huku usafirishaji wa bidhaa ukitatizika kwa miaka mingi.