Wakazi wa kaunti ya Mombasa wamedhihirisha matumani yao ya kubadilika kwa uongozi wa taifa hili kufuatia hotuba ya baba Mtakatifu Papa Francis katika ibada maalum aliyoingoza humu nchini.
Wakizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, punde tu baada ya ibada maalum ya Papa Francis, wakazi hao walisema kwamba hotuba hiyo imewaunganisha wakenya na viongozi wa taifa hili, hivyo basi kiuchumi wa nchi utabadilika.
Wakiongoziwa na Kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni mjini Mombasa Maxwell Masai, wamesema kwamba serikali inafaa kuchukua mfano wa Baba Mtakatifu kuwajibikia majukumu yao vyema ili wakenya kuzidisha uuwiano na utangamano miongoni mwa jamii.
Kulingana na Masai, hatua ya Papa Francis ya kupanda mti katika taifa la Kenya kunaashiria wazi kuwa wakenya wanafaa kutambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili kuepukana na masaibu yanayolikumba taifa hili kila uchao.
Amesema kwamba hatua hiyo italeta wakenya pamoja na kuhakikisha kuwa ujumbe wa amani unazidishwa katika kila sehemu ya taifa hili, huku akiwataka viongozi wa kisiasa, kidini, jamii na mashirika mbalimbali nchini kuzingatia ujumbe wa kiongozi huyo wa dini ya katoliki duniani.
"Tuna matumani kuwa wakenya waliupokea vyema ujumbe wa Papa Francis wa amani na utatuunganisha pamoja, na hatua ya kupanda mti nchi imeonyesha wazi kuwa wakenya lazima tuzingatie mazingira ili tuweze kukabiliana na changamoto za kimazingira," alisema Masai.
Ziara ya Papa Francis inatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa baada ya kukutana na vijana katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi kisha kuelekea nchini Uganda kwa ziara nyengine.