Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa eneo la Vijiweni katika mtaa wa Mtongwe Kaunti ya Mombasa wamelalamikia kusumbuliwa na tumbiri ambao wamekuwa na mazoea ya kuingia kwenye nyumba zao na kuharibu chakula pamoja na vitu vingine vya nyumbani.

Wakazi hao pia wanasema kuwa tumbiri hao huzunguka kwenye paa za nyumba hasa nyakati za usiku, ambapo wakati mwingine hungia na kutoa nguo kwenye mahali zimeanikwa na kuponyoka nazo kwenda msituni.

Wakazi hao, wakiongozwa siku ya Jumapili na Nathan Nyale, ambaye ni kiongozi wa wamiliki nyumba katika mtaa huo, walidai kuwa wanyama hao wamefanya mazoea ya kuingia kwenye majumba yao hasa nyakati hawapo, na wanahofia huenda wakapatwa na maradhi kwa vile wanyama hao hungia na kuchafua maji na hata kukojolea vyakula.

Anadai kuwa tumbiri hao huruka kutoka eneo la kambi ya jeshi wa nevi kwenye mtaa wa Mtongwe na kuingia katika ploti za watu.

“Tumbiri hawa wanaleta kero kwenye mtaa kila mara na wamekuwa wakitusumbua kwenye nyumba, huwezi kuacha nyumba wazi, wala kumuacha mtoto mdogo peke yake kwa sababu baadhi ya tumbiri hawa wakiwa na watoto wao ni wakali na wanaweza hata kumpiga mtoto mdogo au kumdhuru katika harakati za kutoroka wanaposikia sauti ya mtu mzima akiwakaribia,” alisema Nyale.

Wakazi hao walitoa wito kwa serikali kuu kufanya juhudi ili kuwasuluhishia tatizo hilo.