Wakazi katika maeneo ya makazi ya Grand na Soko Mjinga katika mtaa wa Mtongwe eneo bunge la Likoni wanaomba serikali kuu kuwapa usalama katika mtaa huo ambao umekuwa na visa vya mashambulizi kutoka kwa magenge ya uhalifu.
Wakiongozwa siku ya Jumamosi na Emmo Kerah, ambaye ni mkazi wa eneo hilo alisema kuwa kwa siku takriban ishirini zimepita, wakazi wamekuwa wakilengwa na magenge ya majambazi ambao wanalenga hasa wenye maduka ya kuuza bidhaa pamoja na watu wanaoaminika kufanya kazi kubwa.
Kerah alitoa mfano wa kisa cha wiki jana ambapo genge la zaidi ya watu watano waliingia kwenye mtaa huo na kujaribu kumuibia mkazi mmoja mwenye duka mtaani humo ambapo kwa bahati mbaya watu waliweza kugundua njama yao na kupiga kelele.
Majambazi hao alisema kuwa walitoroka lakini walifyatua risasi na kumpiga kifuani mteja mmoja alikuwa akinunua bidhaa kwenye duka hilo.
“Chini ya mwezi wakazi wa hapa wameshambuliwa kama watatu na zaidi na wale wanahusika na kama wanatoka mitaa mingine na huwa wanapewa mwelekeo labda na viongozi wao, sababu mara nyingi wanapojaribu kutoroka wengine hujipata wakiingia katika makazi ya watu na wakiulizwa wanakoishi uonekana hawajui,” alisema Kerah.
Aliomba idara ya polisi kuongeza doria katika eneo hilo hasa nyakati za usiku kuanzia saa moja kesni huo ndio wakati wakora hao huanza shughuli za kutatiza amani.