Mipango ya serikali ya kaunti ya Nyamira kupanua zahanati ya Mwongori na kuifanya hospitali kiwango cha juu huenda ikafanikiwa baada ya wakazi wa eneo hilo kupeana ardhi kwa hiari ili kuwezesha hospitali hiyo kupanuliwa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongozwa na mwakilishi wa wadi ya Mekenene Alfayo Ngeresa, wakazi hao walisema kuwa ufanishi wa kupanuliwa kwa zahanati hiyo utakuwa wa manufaa kwao kwa kuwa watasaidika pakubwa kupata matibabu muhimu karibu na nyumbani.

"Ningependa kuwashukuru watu wetu kwa kuona umuhimu wa mradi huu kwa minajili ya upanuzi wa zahanati hii kwa kutoa ardhi zao kwa hiari kwa kuwa mradi huu ni wa kutufaa sisi sote na haina sababu sisi kuupinga," alisema Ngeresa. 

Kwa upande wake, katibu wa wizara ya afya kwenye serikali ya kaunti ya Nyamira Douglas Bosire aliwashukuru wakazi wa eneo hilo kwa hatua ya kupeana ardhi zao, akiongeza kusema serikali ya kaunti imeweka mikakati kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaimarika kote Nyamira," 

Wizara ya afya kwenye kaunti ya Nyamira ndiyo hupata mgao mkubwa wa pesa na tunahitaji watu wetu kupata matibabu kwa haraka karibu na makwao pasina kusafiri kwenda sehemu za mbali kupokea huduma za matibabu wanazoweza kupata nyumbani kwao, na ningemwomba mwanakandarasi aliyepewa kazi hii kuanzisha upanuzi wa zahanati hii mara moja," alisema Bosire.

Wakazi wa eneo hilo walipeana hekari mbili za shamba kufanikisha upanuzi wa zahanati hiyo.