Wakaazi wa Mzee Wanyama eneo la Pipeline viungani mwa mji wa Nakuru wameelezea changamoto wanazopitia kuwadhibiti wanyamapori haswa nyani, ambao wamekuwa kero katika eneo hilo.
Wakizungumza na mwandishi huyu Jumatatu, wakaazi hao ambao wengi wao ni wakulima wamesema eneo hilo lipo karibu na mbuga ya wanyamapori ya ziwa Nakuru ambako wanyama hao hutoka na kuharibu mimea yao.
“Eneo hili linafaa kuitwa ‘Wanyama’ na wala sio Mzee Wanyama kwa sababu ni wanyama ndio wanatawala eneo hili,” alisema Charles Mwangi, aliyeonekana kukerwa na wanyama hao.
Mwangi, ambaye ni mwakilishi wa wakazi hao, alisema wamekuwa wakiyapeleka malalamishi yao katika afisi za shirika la KWS lakini hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa kuwadhibiti wanyama hao.
Amesema wanyama haina ya nyani wamekuwa wakiyaaharibu mazao yao shambani, jambo ambalo hupelekea wao kwenda hasara.
Hata hivyo, wakazi hao wametaka serikali kupitia shirika la kuhifadhi wanyamapori kuwaondoa wanyama hao kwa kuwa wanawasababishia hasara kubwa kila mwaka.