Viongozi mjini Naivasha sasa wanataka kufanyika kwa mazungumzo baina yao na mashirika mbali mbali yaliyoko eneo hilo ili wakazi waweze kunufaika na rasilimali zilizopo.
Viongozi hao aidha wamesema inasikitisha kuona kuwa wakazi wanataabika licha ya kuwa na rasilimali tele ambazo zingesaidia kuinua hali ya maisha yao.
Haya yameibuka wakati wa mkutano wa viongozi wa muda wa chama kipya cha Jubilee katika hoteli moja mjini Naivasha.
Mwenyekiti wa muda wa chama hicho tawi la Naivasha Ndegwa Ngithiru alisema kuwa eneo la Naivasha halina maji safi ya kunywa licha ya mashirika yaliyoko eneo hilo kutoa maji kwenye milima ya Abadere bila ya kuwagawia wakazi.
“Rasilimali kama vile mvuke ulioko eneo la Olkaria, ziwa letu hapa mjini Naivasha na mbuga za kitaifa za Hellsgate na Longonot zinafaa kutusaidia sisi wakazi wa eneo hili,” alisema Nguthiru, ambaye pia ni mhandisi wa maswala ya maji.