Wananchi wa Kaunti ya Nakuru wameanza kunufaika na shirika lisilo la kiserikali linalotoa msaada kwa jamii bila malipo.
Shirika la Wakfu wa Obama, shirika lililoanzishwa na Marlick Obama nduguye Rais wa Marekani Barrack Obama, kufikia sasa limejenga shule ya chekechea, msingi na ya upili katika eneo la Ngambo katika wadi ya Kapkures.
Akizungumza katika mahojiano, mratibu wa shirika hilo katika kaunti ya nakuru, Margaret Githinji, amesemakuwa kwa sasa shule hiyo iliyokamilika hivi majuzi inatarajiwa kuwachukua wanafunzi toka chekechea hadi darasa la saba huku shule ya upili ikichukua hadi kidato cha tatu.
Bi. Githinji amesema wazazi wanahitajika kujisajili kwa shilingi elfu mbili tu, na baada ya kuwa memba, wanao watasomeshwa hadi chuo kikuu bila malipo.
Mratibu huyo alifichua kuwa wakfu wa Obama utawakilishwa katika maeneo bunge yote ya Kaunti ya Nakuru, huku akitoa mwito kwa wananchi kujisajili.
Wakfu wa Obama, unatoa huduma kama vile elimu bila malipo, afya, ajira kwa vijana na pamoja na kuwajali wakongwe katika jamii.
Kaunti ya Nakuru ndiyo kaunti ya kwanza kunufaika tokana na shirika hili kati ya kaunti zote 47.
Githinji amewaomba wasiojiweza katika jamii kuchukua fursa hii ili kunufaika huku tunapoazimia ruwaza ya 2030.