Wananchi katika Kaunti ya Nakuru wameitaka idara ya afya ya umma eneo hilo kuelezea kwa ufasaha ripoti ya wiki jana kwamba baadhi ya magari yanayouza maji ya matumizi nyumbani yanajishusisha na uzoaji wa siwa inayoenda kutupwa katika uwanja wa Gioto.
Wiki moja iliyopita, afisa wa afya ya umma katika jimbo la Nakuru Samwel King’ori alisema baadhi ya magari hayo yamekuwa yakionekana katika eneo la Gioto yakimwaga uchafu.
Mkaazi mmoja, Irene Mwangi, mmiliki wa chumba cha kusetiri wanafunzi katika mtaa wa Banga, alisema afya ya wakazi wa kaunti hiyo ambayo miezi kadhaa ilikumbwa na mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu, imo hatarini kama habari hizo ni za kweli.
Naye Geofrey Maina, kutoka Kaptembwa, ambaye huadhirika sana wakati wa mafuriko alisema wamekuwa wakilalamika uwanja huo wa kutupia taka uondolewe maeneo ya juu ya mji wa Nakuru bila mafanikio.
“Kukinyesha hapa Kaptembwa hakukaliki tena kwa sababu ya uvundo wa uchafu wa choo unaotoka Gioto na Gk prison,” alisema Maina.
Kulingana na King’ori, uchunguzi wa visa hivyo umeanzishwa ili kufungulia mashtaka watakaopatikana wakifanya makosa hayo, huku akidokeza kuwa afisi yake inaweka mikakati ya kutoa leseni kwa magari yanayofaa kusafirisha maji safi katika jimbo hili.
King’ori alidokeza kuwa wiki mbili zilizopita, visa vitatu vya ugonjwa kipindupindu viliripotiwa katika jimbo, viwili kutoka Mogotio na kimoja kutoka Naivasha.