Kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini, wakulima kwenye kaunti ya Nyamira wamehimizwa kuhifadhi maji ya mvua kwa minajili ya kujiandaa kukabili msimu wa kiangazi mapema mwakani.
Akihutubia wanahabari afisini mwake mapema Ijumaa, mkurugenzi wa shirika la ukuzaji na uimarishaji wa kilimo tawi la Nyamira Yuvinalis Orenge aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kuhifadhi maji kwa wingi kwa kuwa huenda ikawa vigumu kupata maji pindi tu msimu wa mvua utakapokamilika.
"Nawahimiza wakazi kuchukua hatua ya kuhifadhi maji hasa kwenye msimu huu wa mvua kwa kuwa itakuwa vigumu kupata bidhaa hiyo hasa kwenye msimu wa kiangazi ujao," alihimiza Orenge.
Akizungumzia swala la kusaidia makundi mbalimbali ya wakulima wanaokuza mboga za kienyeji, Orenge alisema tayari shirika hilo limesambaza mitambo ya kukausha mboga katika kila wadi kaunti ya Nyamira, huku makundi mbalimbali yakipokezwa mafunzo ya jinsi ya kukausha mboga hizo zitakazosaidia katika msimu wa kiangazi.
"Tayari tumesambaza mashine za kukauza mboga katika kila wadi Nyamira ili kuwasaidia wakulima kukausha mazao yao hasa mboga kwa minajili ya kuwasaidia kuweka mboga hizo zitakazowasaidia kwenye msimu wa kiangazi," aliongezea Orenge.