Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini inapoendelea na shughuli za usajili wa wapiga kura kote nchini, mwanaharakati wa haki za kibinadamu Aggrey Angwenyi amejitokeza kuwahimiza wananchi katika kaunti ya Nyamira kuhakikisha kuwa wamesajiliwa. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu katika shule ya msingi ya Nyamaiya siku ya Jumatatu wakati wa kuwapokeza zawadi wanafunzi waliofanya vyema kwenye mtihani wa kitaifa wa darasa la nane mwaka jana, Angwenyi alisema kuwa sharti wananchi wajitokeze kusajiliwa kama wapiga kura iwapo kwa kweli wanataka kubadilisha hali ya uongozi kwenye uchaguzi mkuu ujao. 

"Sharti sisi wananchi tulio hitimu miaka 18 na zaidi tujitokeze kusajiliwa kama wapiga kura kwa maana kura tu ndio silaha itakayotuwezesha kuwaondoa mamlakani viongozi wasio wachapa kazi," alisema Angwenyi. 

Angwenyi aidha aliongezea kwa kuwahimiza wananchi kutoruhusu kununuliwa na baadhi ya wanasiasa ili kwamba wasipige kura kwenye uchaguzi mkuu ujao. 

"Kuna ripoti kwamba baadhi ya wanasiasa wanaohofia kushindwa kwenye uchaguzi mkuu ujao wameanza kununua vitambulisho kutoka kwa wapiga kura ili wasiwe na uwezo wa kupiga kura mwaka ujao, ila ni himizo langu kwenu kutokubali kuuza vitambulisho vyenu kwa kuwa hiyo ndio silaha ya kipekee mnaweza tumia kubadilisha uongozi nchini," aliongezea Angwenyi.