Wakazi wa Nyansiongo wamejitokeza kuisifia serikali ya Kaunti ya Nyamira kwa kuanzisha mradi wa kukarabati barabara ya kutoka Nyandoche Ibere kuelekea katika eneo la kibiashara kule Nyansiongo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu wakati wa kufungua rasmi mradi huo siku ya Jumanne mwakilishi wadi ya Nyansiongo Jackson Mogusu alisema kuwa pindi tu barabara hiyo itakapokamilika, wakazi wa eneo hilo hasa wakulima watakuwa na urahisi wa kusafirisha mazao yao hadi sokoni. 

"Ningependa kuishukuru serikali ya kaunti hii kwa kujitolea kwake kuhakikisha kuwa barabara hii imekarabatiwa kwa maana sasa wakulima wengi wanaouza maziwa ambao kwa muda wamekuwa wakinishtumu sasa watapata afueni ya kusafirisha maziwa yao kwa urahisi," alisema Mogusu. 

Mogusu aidha aliwataka wanakandarasi waliopewa kazi ya kuikarabati barabara hiyo kuhakikisha kwamba wanakamilisha mradi huo kwa njia inayostahili na kwa haraka. 

"Itakuwa vizuri iwapo wanakandarasi waliopewa kazi ya kukarabati barabara hii kumaliza mradi huu kwa haraka ili shughuli za kawaida hasa hasa za kibiashara zirejelewe kama kawaida," aliongezea Mogusu.