Shughuli za kawaida zimesitishwa mjini Mombasa baada ya wakazi zaidi ya 200 kutoka eneo la Owino Uhuru eneo bunge la Jomvu kuandamana hadi katika afisi za Mamlaka ya Mazingira nchini NEMA kulalamika kutotibiwa kwa eneo hilo.
Wakiongozwa na mkurungezi mkuu wa shirika la kupigania haki za kimazingira la ‘Centre for Justice and Environmental Action’ Bi Phyllis Omido, wakazi hao wamesema kwamba zaidi ya miaka mitano sasa tangu wapiganie haki za wakazi hao, serikali haijajitokeza kuwaokoa wakazi kufuatia kuathirika na sumu ya madini ya vyuma.
Akiongea na wanahabari nje ya afisi za mamlaka ya kimazingira mjini Mombasa siku ya Alhamisi baada ya maandamano hayo, Omido amesema kwamba mamlaka ya Nema imeonekana kukosa kuwajibikia majukumu yake, na kuacha wakazi kupoteza maisha yao.
Omido aidha amesema kwamba zaidi ya wakazi 300 kati ya wakazi elfu tatu wamepatikana wameathirika na sumu hiyo ya madini ya vyuma katika eneo hilo, na akasema kwamba kuna haja ya serikali kuu na zile za kaunti kuingilia kati swala hilo na kuwanasua wakazi.
"Tunashindwa kuielewa serikali pamoja na mamlaka ya kimazingira kwa kutotemmbela eneo la Owino Uhuru na kutibu eneo lile lililoena sumu ya madini ya vyuma, na wakazi wengi wameathirika. Tunataka watume maafisa wa afya kuwapima wakazi ili kutambua viwango vya sumu ya madini ya vyuma iliyo ndani ya miili yao," alisema Omido.
Hata hivyo, juhudi za kuwasiliana na afisa mkuu wa mamlaka hiyo ya Nema mjini Mombasa ziligonga mwamba pale afisa huyo alipokwepa wanahabari.