Serikali ya kaunti ya Nyamira imeombwa kulima vitufe na matuta kwenye eneo la Raitigo ili kusaidia uharibifu wa mimea kutokana na mvua kubwa ya Elnino inayoendelea kunyesha.
Akihutubu siku ya Alhamisi kwenye hafla ya umma iliyoandaliwa katika sehemu hiyo, msemamaji wa wakazi wa eneo hilo Peter Mosoku alilalamikia kutojitolea kwa serikali ya kaunti ili kuwasaidia kukabili athari za El-nino katika eneo hilo.
“Eneo hili ni mojawapo ya sehemu inayochangia pakubwa kwenye kuimarisha hali ya uchumi kwenye kaunti ya Nyamira, na inashangaza kuwa serikali haijafanya lolote ili kutusaidia kuzua kusombwa kwa mimea yetu na ndio maana tunahitaji matuta na vitufe kulimwa kwenye barabara kuu za eneo hili ili kupunguza athari za kusombwa kwa mimea,” alisema Mosoku.
Wakazi hao aidha waliishtumu serikali ya kaunti ya Nyamira kwa kusema kuwa imekuwa ikijikokota kuwasaidia kurekebisha hali hiyo, hata baada yao kuwasilisha lalama zao kwa serikali kupitia kwa mwakilishi wa sehemu hiyo Jackson Mogusu.
“Tunajua kuwa serikali ya kaunti ya Nyamira ilikuwa imetenga kiwango flani cha fedha ili kukabiliana na madhara ya El-nino lakini ingali serikali ya kaunti inajikokota kusikia kilio chetu. Hata baada ya kuzungumza na mwakilishi wadi hii Jackson Mogusu aliyetubithishia kuwasilisha lalama zetu kwa gavana Nyagarama bado hatujapata msaada,” alihoji Mosoku.
“Ni jambo la kuhuzunisha kuwa hamna hatua yeyote iliyochukuliwa hata baada ya kuwasilisha lalama zetu kwa kamati ya kuthibiti majanga,” alisema Mosoku.