Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Riooga kwenye eneo bunge la Kitutu Masaba wamelalamikia vikali hatua ya wadumishaji usalama vijijini kujitwika majukumu yasiyokuwa yao.
Wakazi hao walioongozwa na diwani wa zamani wa Gesima Mokaya Nyambaoni walitishia kumwandikia barua kamishna wa kaunti ya Nyamira Josphine Onunga kulalamikia hatua ya wadumishaji usalama hao kujitwika majukumu ya polisi, ikiwa naibu chifu wa eneo hilo hatowakanya.
“Kenya ni nchi inayoongozwa na sharia, na kamwe hatutakubali watu waliopewa majukumu ya kudumisha usalama vijijini kuanza kufanya kazi za maafisa wa utawala, tunamtaka naibu chifu wa eneo hili kutupa sababu ya watu hao kuwachapa na kuwaumiza vibaya vijana watano,” alisema Nyambaoni.
Nyambaoni aliongeza kwa kumsihi kamishna wa kaunti hiyo Josphine Onunga kuwafuta kazi maafisa wa utawala ambao wamekuwa na mazoea ya kuwahangaisha wenyeji kwa kuitisha hongo kila mara wanapowapata wahusika na hatia.
“Kuna maafisa wa utawala ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakazi kwa kuwaitisha hongo kila mara wanapowapata wahusika na hatia, na tunamtaka kamishna Onunga kuwaachisha kazi mara moja kwa kuwa maafisa kama hao wanaenda kinyume na sheria za nchi," aliongezea Nyambaoni.
Haya yanajiri baada ya wadumishaji usalama vijijini katika eneo hilo kuwachapa na kuwaachia majereha makali vijana watano kwa kuwapata wakiwa wamechelewa kufika nyumbani siku ya Jumapili.