Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi wa kaunti ndogo ya Rongai wameombwa kuwaripoti watu ambao wanaendeleza uchuuzi wa nyama ya mbuzi na ngombe.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, daktari wa mifugo eneo hilo Martin Karite alisema kwamba, kuna watu ambao wanauza nyama hiyo asubuhi na mapema, nyama ambayo haijakaguliwa na daktari kuwa nzuri kwa matumizi.

“Tumefanya utafiti na tumegundua kuwa watu wanaouza nyama ambayo haijakaguliwa wanafanya shughuli hiyo majira ya asubuhi na mapema ili kukwepa maafisa wa afya,” alisema Bw Karite.

Ameongeza kuwa watu ambao wanaendelea kununua nyama hiyo wanajitia kwenye hatari ya kupatwa na maradhi ambayo hutoka kwa mifugo hadi kwa binadamu.

“Ningeomba wakaazi wa eneo hili wajitahadhari sana maanake nyama ambayo haijakaguliwa inaweza kusababisha maradhi yanayoambukizwa kutoka kwa mifugo hadi kwa binadamu,” aliongeza Bw Karite.

Badala yake amewataka wananchi kununua nyama kwenye maduka ya nyama na kuhakikisha imewekwa muhuri wa kuonyesha kuwa imekaguliwa na daktari aliyeidhinishwa.

Aidha alisema kuwa watakaokamatwa wakiendeleza uchuuzi wa nyama watachukuliwa hatua kali za kisheria.