Kampuni ya uwekezaji ya Cytonn Investments Ltd imezindua mradi wa ujenzi wa nyumba zaidi ya 400 za kupanga katika eneo la Ruaka, Kaunti ya Kiambu.
Mradi huo wa Alma Apartments, ambao unatarajiwa kugharimu takriban shilingi bilioni tatu, utasimama kwa ardhi ya hekari 4.18 huku nyumba zake zikitarajiwa kuuzwa kuanzia shilingi milioni 5.5.
"Alma Apartments ambayo itajengwa kwa ujuzi wa kisasa ni muafaka kwa vijana wanaoanza familia za kisasa na itapatikana kwa rumu moja au mbili za malazi," alisema James Maina, mwanachama wa bodi ya Cytonn Investments Ltd.
Aliongeza, "Miundo mbinu na miundo misingi itakayopatikana hapa ni kama vile maduka, hospitali, klabu, shule ya chekechea, kidimbwi cha kuogelea na kadhalika."
Mradi huo unatarajiwa kuwapa zaidi ya watu 1,000 ajira, wengi wao wakiwa vijana wa Kaunti ya Kiambu.