Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Zaidi ya wakazi 300 wa Seguton mjini Baringo waliandamana Jumatano asubuhi  kulalamikia hali duni za barababara kwenye maeneo hayo.

Wakazi hao walisema kuwa hali ya barabara ya Seguton kuelekea Timboroa ni duni, hali inayosababisha mazao yao kuozea shambani na kuathiri biashara ya pikipiki.

“Kusafirisha mazao kwa soko imekuwa changamoto kwetu kwani magari na hata mapikipiki hayapiti kwenye barabara hiyo,” Daniel Karigo, mmoja wa wakazi alisema.

Wakazi hao walilalamikia kutopata habari ya kutengenezwa kwa barabara hiyo kwenye Kaunti, ingawa wanaseme wamewasilisha malalamishi yao.

“Ni vibaya sana kwani hawajatuarifu kuhusu jambo lolote tangu tulipowasilisha malalamishi yetu miezi kadhaa iliyopita. Hata hivyo waliposikia tunaandamana asubuhi walituarifu watakuja kutatua mashida zetu lakini mpaka saa huu hakuna mwenye amejitokeza,” Karigo aliongeza.

Wengi wa wakazi hao walilalamikia visa vya kina mama wajawazito kujifungua kwenye barabara hiyo wanaposafirishwa hospitalini.

“Visa vya kina mama kujifungua kwenye barabara vimeongezeka sana kwani barabara hii haipitiki, hali inayowafanya wakazi wabebe wajawazito wenyewe mpaka hospitali,” alisema mkazi mwingine.