Wakazi waliopewa hati miliki na Rais Kenyatta katika shamba lenye utata la Waitiki sasa wanadai kuwa vyeti hivyo vina wakanganyana baada ya kugundua kuwa vina majina yao pamoja na jina la benki moja ya humu nchini.
Wakizungumza na mwanahabari huyu mapema siku ya Jumatatu, wakazi hao wakiongozwa na Nusra Mwinyi walisema kuwa wameshindwa kuelewa kwanini jina la benki hiyo limejumuisha kwenye vyeti hivyo.
Mwinyi anasema kwa sasa wanaogoga kuvitumia vyeti hivyo hadi watakapopewa ufafanuzi zaidi kwani wanahofia huenda benki hiyo ikapiga mnada mali zao iwapo watashindwa kulipa ada ya umiliki walivyoagizwa na Rais Kenyatta.
''Jameni tuko gizani hapa, vyeti tumepewa lakini hatuelewi kwanini jina la hii benki pia limejumuisha. Hatujui kama ardhi ni yetu ama ni ya benki hiyo,'' alisema Mwinyi.
Mwinyi vilevile aliwataka viongozi wa serikali kuu, viongozi wa kaunti ya Mombasa na maafisa wa ardhi kujadiliana kuhusu uwezekanao wa kuondoa ada wanayotakiwa kulipa, huku akisema wengine wao wako chini kimapato.
Hata hivyo, kauli yake iliibua hisia kinzani pale mkazi mwingine kwa jina Janet Mbete alipowahimiza wenzao kujituma ili kulipa ada hiyo huku akiitaja kuwa ya kiwango cha chini ambayo kila mkazi anaweza kumudu.
Siku ya Jumamosi, Rais Kenyatta aliwapa hati miliki takribani maskwota 5,000 wanaoishi katika shamba la Waitiki na kuwataka kuilipia ada ya shilingi 1,000 kila mwezi kwa muda wa miaka 12 ili kufidia pesa zilizotumika kumlipa Waitiki.