Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wa eneo bunge la Nakuru magharibi wamehakikishiwa kuwa serikali ya Jubilee iko tayari kuimarisha eneo hilo kwa kuendeleza miradi mbalimbali ili kuimarisha maisha ya wananchi licha ya kuwa ngome ya chama pinzani cha Cord.

Mbunge wa eneo hilo Samuel Arama, ambaye pia aliteuliwa na tiketi ya chama cha Cord, alielezea wananchi kuondoa hofu yoyote na kutofautiana na masuala ya kisiasa ambayo hayaleti utangamano.

"Serikali ya Jubilee iko mbioni kuboresha maisha ya kila mmoja kwa kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo ya uchumi ili kuleta maendeleo na umoja kote nchini. Hivyo basi nawasihi mtofautiane na siasa ambazo hazileti maendeleo yoyote nchini," Arama alielezea.

Arama alikuwa akizungumza siku ya Jumamosi katika sherehe ya kuhitimu kwa vijana wa shule ya upili ya Menengai. 

Mbunge huyo pia aliwahakikishia wakazi wa eneo hilo kuwa Jubilee itatimiza ahadi zake kwa wananchi kabla ya uchaguzi ujao, huku akipongeza Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa kazi wanazofanyia wananchi.

"Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto wamekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kila maeneo yanapata usaidizi kutoka kwa serikali. Huu ni wakati wa kuungana pamoja na kuboresha maisha ya wananchi," Arama aliongezea.