Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi kutoka eneo la Bahati, Nakuru wamekashifu uuzaji na unywaji wa pombe haramu katika eneo hilo, swala wanalotaja linazidi kurejelewa kila kuchao licha ya kupigwa marufuku na rais Uhuru Kenyatta mapema mwaka huu.

Wamedai kuwa kuuzwa kwa pombe hiyo kunaruhusiwa na maafisa wakuu wa eneo hilo, ambao wanadaiwa kushirikiana na wapishi wa pombe hizo, hatua inayotajwa kuwa chanzo cha kuwepo kwa pombe hizo.

Wakiongea Jumatatu adhuhuri mjini Nakuru wakiongozwa na aliyekuwa kaimu mwenyekiti wa TNA Dkt Abdul Noor, wakazi hao wametaka kuchukuliwa hatua kwa maafisa wanaotajwa kutepetea katika utendakazi wao, huku wakilalamika kuwa licha ya baadhi ya wapishi kunaswa baada ya shinikizo kutoka kwa wananchi, wengi wao hukosa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka kwa kuwa ufisadi umekithiri katika baadhi ya maafisa wa serikali wanaoshughulikia swala la pombe haramu.

“Watu wakipelekwa katika kituo cha polisi cha Bahati wanaachiliwa kwa shilingi 500, kwa sababu ya hongo iliyokithiri katika idara ya polisi, ikiwa ufisadi itaendelea hivi, basi hatuwezi kuafikia lolote katika vita vya kupigana na pombe haramu,” akasema Noor.

Wakati uo huo, Noor amemtaka kamishna wa jimbo la Nakuru Josua Nkanatha na Gavana Kinuthia Mbugua kuchunguza visa hivyo na kubaini jinsi leseni za vituo vya kuuza pombe haswa vilabu zinavyotolewa, ikizingatia kuwa zoezi husika lilisitishwa jimboni hadi pale mwelekeo utakapotolewa.

“Sisi tunamwomba Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua, yeye ni mtu anajua sheria kabisa maanake alikuwa katika idara ya polisi kwa muda murefu, kwa sasa anajua ofisi yake imefunga leseni zote za baa katika kaunti ya Nakuru, lakini tunataka kumfahamisha kuwa kuna watu wanauza pombe na leseni zilifungwa," akaongeza Noor.

Haya yanajiri huku kina mama katika mengi ya maeneo jimboni wakitaja upishi huo kurejelewa, huku wakihofia majanga kama ya awali yanayoletwa na pombe haramu yaliyokumba wapendwa wao kurejea tena.