Huku mvua ikiendelea kuponda mitaa ya makazi katika Kaunti ya Mombasa, wakazi wa eneo la Likoni wameishutumu serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa kuwatenga katika kuwafanyia ukarabati wa miundomsingi.
Wakiongozwa na mzee wa mtaa wa Kiwerera Abdi Buro siku ya Alhamisi, wakazi hao walisema kuwa mvua ambayo imeanza kunyesha wiki hii tayari imewatia hofu kuwa huenda kukashuhudiwa hasara kubwa sana, huku wakitoa mfano wa mvua ambayo imenyesha siku ya Jumatano usiku na kuingia katika nyumba zao.
Wakazi hao walionyesha kutoridhika kuwa na mipango ya kaunti hiyo ikizingatiwa kuwa kuna hela za masuala ya dharura kama elnino zilizotengewa kila kaunti kote nchini kukabiliana na mvua hiyo, na kushangaa ni vipi idara husika iliweza kufanya ukarabati katika maeneo ya makazi yaliyo katika kisiwa ambapo wanaoishi kwenye maeneo hayo ni watu wanaojiweza.
“Si tayari kuna mamilioni ya pesa zilitengwa kufungua mifereji, mabomba ya kupitisha maji ya siweji na uchimbaji wa mitaro, lakini hapa kwetu hatujaona chochote kikifanyika, na mvua ndio hii imeanza kunyesha na mathara tayari unayaona, serikali sharti iwajibike na kuchunguza miradi hii,” alisema mzee Abdi.
Walitoa wito kwa serikali ya kitaifa kuanza kufuatilia jinsi pesa hizo zinatumiwa, na kudai kuwa huenda pesa zimetumiwa vibaya na baadhi ya maafisa na miradi lengwa bado haijatekelezwa.