Wakazi katika eneo la Mkomani katika eneo bunge la Kisauni wamelalamikia pesa nyingi wanazotozwa vijana wa bodaboda pamoja na vijana wa mtaa ambao wanawavusha kutoka eneo la barabara kuenda katika maeneo yao ya makazi.
Wakazi hao wamesema kuwa tangu wiki jana, njia nyingi za kuingia katika makazi zimejaa na kufungwa kwa kutwama kwa maji ya mvua ambayo inaendelea kunyesha, na juhudi zao za kutumia pikipiki wakati wanapoenda na kutoka kazini zimewaponza kwenye mikono ya wanabodaboda ambao wanawaomba katika ya shilingi 50 hadi 100 kuwavusha kwenye njia hizo ambazo walisema hazipitiki kwa sababu ya maji.
Wakiongea siku ya Jumapili na mwaandishi huyu katika eneo hilo, kupitia kwa mwenyekiti wa wakazi wa mtaa huo, Taru Kondo, walisema kuwa si haki hata kidogo ikizingatiwa kuwa wengi wa wakazi katika eneo hilo ni vibarua au hufanya shughuli za kazi yenye mapato madogo.
Kwa mujibu wa mzee Kondo, vijana hao hujitolea kuwabeba kwa hela ambazo wanaelewana lakini baadaye wanapowafikisha katikati ya maji hayo huwageuka na kuwataka kuongeza pesa au wawachilie, hali ambayo mzee huyo alishtumu vikali na kuomba idara ya kushughulikia masuala ya dharura kutembelea eneo hilo na kukarabati miundomsingi ili kuepusha kutokana na visa hivyo.