Baadhi ya wakazi katika kaunti ya Nyamira wamejitokeza kulalamikia vikali hatua ya gari la kliniki tamba katika kaunti hiyo kuwa katika eneo la maegezo miezi kadhaa baada ya mke wa Rais Kenyatta kulipokeza serikali ya kaunti hiyo.
Kwenye mahojiano ya kipekee siku ya Jumatatu wakazi hao walisema wanashangazwa ni kwa nini gari hilo lingali linaegezwa nje ya hospitali, ilhali linatarajiwa kuwasafirisha kina mama wanaotaka kujifungua hadi kwenye hospitali hiyo.
“Tunashindwa ni kwa sababu gani gari la kliniki tamba lingali kwenye maegezo nje ya hospitali kuu ya Nyamira ilhali kuna kina mama waja wazito vijijini wasio na uwezo wa kusafiri hadi kwenye zahanati na hospitali mbalimbali ili kujifingua,” alisema Joel Orang'o, mmoja wa wakazi wa Nyamira.
Orang'o aidha alimtaka waziri wa afya katika kaunti hiyo Gladys Momanyi kuweka mikakati ya kuhakikisha gari hilo linawashughulikia kina mama wajawazito kwa haraka la sivyo lirejeshwe kwa wakfu wa Weymss Foundation.
“Inafaa iwekwe ratiba ya jinsi gari hili la kliniki tamba linafaa kutekeleza shughuli zake na hilo ni jukumu la waziri wa afya na iwapo hilo halipo kwenye mipangilio yake yafaa gari hilo lirejeshwe kwa wahisani wa wakfu wa Wemyss," aliongezea Orang'o.