Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa mtaa wa Ngesha katika wadi ya Kabatini wamelalamikia ongezeko la ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Hii ni baada ya mtu mmoja kuuawa kinyama alipokuwa akirejea nyumbani kwake usiku wa kuamukia Jumamosi wiki iliyopita.

Kulingana na wakazi hao, George Waweru ambaye alikuwa mfanyikazi wa kampuni ya kuzalisha umeme kutumia mvuke ya GDC aliuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kupatikana kichakani.

Mshirikishi wa mpango wa Nyumba kumi katika eneo hilo Onesmus Mwai alisema kuwa makundi ya wahalifu yamekita kambi katika eneo hilo, na wanashiriki wizi wa kutumia mabavu.

Akiongea na mwandishi huyu, Mwai alisema kuwa wahalifu hao wanawalenga watu walio na pesa.

"Juzi wamemuua kijana mdogo sana hapa chini na wakachukua pesa alizokuwa nazo, na hicho sio kisa cha kwanza. Hapa hatuna usalama kabisa na tunahofia hata kutembea nyakati za usiku," alisema Mwai.

"Tungewaomba maafisa wa polisi kutoka Bahati ama wale wa Nakuru kaskazini watusaidie kuwanasa wahalifu hao ambao ni vijana wadogo sana," aliongeza.

Mwezi Disemba mwaka jana, mama mmoja aliuawa na watu wasiojulikana alipokuwa akitoka benki kutoa pesa za kuwalipa wafanyikazi wake.

Mwai aliwalaumu baadhi ya wahudumu wa bodaboda katika eneo hilo kwa kushirikiana na wahalifu katika eneo hilo na kuwaonya kuwa siku zao zimehesabika.

"Kuna vijana fulani hapa wanawasaidia hao wahalifu kufanya uhalifu wao, lakini tumewatambua na majina yao tumepeana kwa polisi," alisema Mwai.