Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Watu wanaotumia kivuko cha Likoni pamoja na wakazi wa eneo la Railways katika jiji la Mombasa wamelalamikia kushambuliwa na genge la vijana linalotekeleza uhalifu katika eneo hilo nyakati za usiku.

Wakiongea na mwandishi habari huyu siku ya Jumatano katika eneo hilo, wakazi hao walisema kuwa zaidi ya vijana ishirini wamekuwa wakijificha kwenye vibanda vya kuuza nguo na viatu vilivyo karibu na barabara na kuwavamia wapiti njia hasa nyakati za jioni wakati watu wengi wanarudi nyumbani kutoka kazini.

Veronica Malkah, ambaye amekuwa akitumia njia ya reli akielekea kazini amedai kuibiwa simu wiki jana na wakora hao, ambapo walimtishia alipojaribu kupiga kelele na imembidi kuanza kutumia njia nyingine baada ya uhalifu huo.

“Waliniibia simu pamoja na mapeni kidogo niliokuwa nayo, lakini nashukuru Mola hawakunijeruhio. Si mara ya kwanza wanafanya hivyo, siku nyingine walitukimbiza mimi na rafiki yangu lakini tukaepuka, naiomba idara ya polisi kulishughulikia suala hilo haraka sana na kuwashika wahusika,” alisema mkazi huyo.

Mwanaidi Hamisi alisimulia kwa machungu jinsi alivyoingia kwenye mtego wa wahuni hao na kumpiga na walimnyanganya hela zote alizokuwa ameuza kutoka biashara yake ya matunda na mboga za mchicha.

Hata hivyo, wengi wa wakazi hao waliikashifu idara ya usalama nchini kwa kukosa kuwapa usalama wa kutosha katika eneo hilo na kutaka doria kuwekwa zaidi.