Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi pamoja na watumizi wa kivuko cha Likoni wamelitaka shirika la feri nchi kuwa na kikosi maalum cha kupiga mbizi, ambacho kitakuwa kinaokoa watu ambao wamekuwa wakijirusha kwenye Bahari Hindi kwenye siku za hivi karibuni.

Wakazi hao ambao waliongozwa na mzee wa mtaa wa Samaki eneo la Kiwerera Likoni, Athman Bhore siku ya Jumamosi walisema kuwa shirika la feri bado halijajiandaa kikamilifu katika masuala ya dharura, haswa ikizingatiwa kuwa watu wamekua wakijirusha katika maji makuu ya bahari huku, wengine wakiwa wanatumbukia ndani ya maji kwa kujaa sana karibu na mlango wa kuingilia.

Mzee Bhore alitoa mfano wa visa ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa akitoa mfano wa mama mmoja ambaye alitaka kujitoa uhai kwa kujirusha baharini wiki jana, pamoja na kisa cha Ijumaa ambapo inadaiwa mwanaume mmoja alijirusha kwenye bahari muda mchache tu baada ya feri hiyo kuanza kuondoka kwenye eneo la kupakia na kudondosha magari na watu.

“Kisa cha jana (Ijumaa) kilikuwa kama cha tatu chini ya mwezi mmoja ambapo uokozi umekuwa ukitolewa na kikosi cha usalama cha majini cha bandari, ningependa kuona shirika la feri licha ya kuwa na changamoto nyingi liwe na kikosi chake maalumu cha kuokoa maisha ya watu kama hawa ambao labda wamebanwa na mawazo mengi kwa sababu ya changamoto za maisha,” alitoa wito mzee huyo.