Wakazi wa eneo la Kiwerera, huko Likoni katika Kaunti ya Mombasa wanalalamikia kuvamiwa na wadudu aina ya kunguni ambao wanasema wanawakosesha starehe ya kulala.
Wakazi hao, wakiongozwa na Siro Kalu siku ya Jumatano walisema kuwa wamejaribu kila namna na kubuni mbinu za kuwaua kunguni hao lakini wanaendelea kuongezeka, na kuitaka wizara ya afya kupitia idara ya afya ya umma kuingilia suala hilo kati na kuwapa dawa mwafaka ya kuwaangamiza kunguni hao, ambao walidai wanaendelea kuzaana na huenda wakasambaa na kuenda kila nyumba za wakazi.
Siro alitoa hofu kuwa wadudu hao huenda wakawasababishia maradhi ya ngozi na maradhi mengine kama ya anemia, ambayo ni hatari iwapo hakutachukuliwa hatua ya haraka mapema ya kushughulikia swala hilo.
“Hawa kunguni wanatusababishia masaibu mengi yakiwemo ukosefu wa kulala, aibu huwezi hukaleta mgeni katika nyumba sababu wanatembea ovyo kwenye vitambaa na kitanda sisi kama wakazi tumejaribu kutafuta aina zote za dawa na sumu ili kuwaulia lakini wapi, tunaomba serikali au mtaalam yeyote ambaye ana fahamu ya dawa mwafaka ya kuwaangamiza wadudu hawa,” alisema mkazi huyo.
Alidai kuwa watoto, kwa kiwango kikubwa wamejipata katika hatari ya kuambukizwa maradhi ikizingatiwa kuwa ndio wanakua.