Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wananchi wameonywa dhidi ya kuishi kwenye majumba mabovu ambayo hayajafanyiwa ukarabati ili kuepuka majanga zaidi kutokea.

Onyo hili limetolewa na shirika la Msalaba Mwekundu kaunti ya Mombasa ambapo limewashauri wakazi kuwa waangalifu hasa wakati huu wa msimu wa mvua ili kuepukana na majanga, huku wakazi wanaoishi maeneo ya mabonde wakishinikizwa kuhamia maeneo ya juu.

Kulingana na shirika la msalaba mwekundu mjini Mombasa, zaidi ya nyumba 15 zimo hatarini na tayari wakazi wameambiwa wahame eneo hilo ambalo liko na zaidi ya wakaazi 50,000.

Kauli hii inajiri baada ya mtu mmoja kufariki huku wengine wawili wakijeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba usiku wa kuamkia siku ya Jumatano katika mtaa wa Moroto, eneo la Tudor, mjini Mombasa.

Kulingana na Christine Nzilani, afisa katika shirika la msalaba mwekundu tawi la Mombasa, ukuta huo ulishindwa kujihimili kutokana na mvua nyingi iliyoshuhudiwa siku ya Jumatatu huku akisisitiza umuhimu wa wakazi katika eneo hilo kuhama.

Gabriel Mwashigadi, mmiliki wa nyumba hiyo alisema watu hao wamekuwa wakiingia nyumba hiyo usiku wa manane licha ya onyo la kuporomoka kwa nyumba hiyo kutolewa.

Na kwa mujibu wa chifu wa eneo hilo Halima Kulola, muda wametoa onyo kwa wakazi wanaoishi katika nyumba zenye hatari ya kuporomoka lakini baadhi wanapuuza huku akitoa onyo kwa wakaazi wa eneo hilo kutahadhari.