Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi katika eneo la Kibuyuni B katika wilaya ya Likoni wameipongeza serikali ya kaunti kwa kuanza harakati za kupunguza jaa la taka ambalo limekuwa kero kwa wakazi hao kwa muda sasa.

Wakazi hao ambao walijawa na furaha kufuatia serikali ya kaunti kuanza kutuma magari ya kuzoa taka kutoka eneo hilo baada ya wao kulalamika kwa zaidi ya miezi miwili walisema kuwa wapo tayari sasa kufanya kazi na serikali ya kaunti, na kuitaka serikali hiyo kuweka juhudi zaidi.

Wakiongozwa na Salim Mwalughange siku ya Jumapili, wakazi hao walisema kuwa wangependa kuwaona wazoa taka katika sehemu hiyo angaa kila wiki ili kuepusha kuongezeka kwa taka ambazo mara nyingi hukaa mahali hapo na kuzua arufu mbaya.

Wameitaka serikali ya Gavana Joho kuwahusisha vijana wa eneo hilo kwenye miradi kama njia moja ya kuwapa kazi ili kujiendeleza kimaisha.

“Tunamwomba gavana wetu Joho ajaribu kututafutia miradi ambayo itatufaa kiuchumi kwa vile vijana wa eneo hilo wana uwezo, na ningependa kushukuru serikali yake kwa kuwajibikia jaa hili ambalo limekuwa kero kwa muda mrefu,” alisema mkazi huyo.

Jaa hilo limekuwa na mzozo baina na mwekezaji mmoja ambaye inadaiwa kuwa mwenye kipande cha ardhi hiyo, na wakazi wa Kibuyuni ambapo kwa wakati mmoja wakazi hao walitishia kuandamana ili kushinikiza hatua kuchukuliwa dhidi ya jaa hilo na mmiliki wa kipande hicho.