Mwanasiasa katika eneo bunge la Kitutu Chache kusini Samuel Omwando amewaomba wakazi kutokubali kudanganywa na wanasiasa kuhama hadi vituo tofauti ili kujiandikisha kama wapiga kura katika vituo hivyo.
Kulingana na Omwando, kila mkazi yuko na uhuru wa kujisajili kama mpiga kura katika kituo chochote anachohitaji kando na kusawishiwa na wanasiasa kushika kadi za kura katika vituo tofauti.
Akizungumza siku ya Jumanne katika eneo la Bogisero, eneo bunge la Kitutu Chache kusini, Omwando alidai kuwa kuna baadhi ya wanasiasa ambao wanahitaji kudanganya wakazi wengine kuchukua kura katika vituo tofauti ili kupata afueni ya kupata uungwaji mkono katika uchaguzi ujao.
“Mwanasiasa asiwadanganye kushika kura katika vituo tofauti kama ni kujisajili jisajili katika wadi yako na katika eneo bunge lako, haya mengine ya kuhamishwa hadi eneo bunge lingine au wadi ingine hatutakubali,” alisema Omwando
“Ikiwa unahitaji kubadilisha uongozi katika mahali uliko sharti ujiandikishe kama mpiga kura katika eneo lako na msikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa kuenda kujisajili kwingine hayo hatutakubali,” aliongeza Omwando.
Wakati huo huo, Omwando aliomba wale wote wanaojiandikisha kuwa wapiga kura wakati wa uchaguzi ujao utakapofika ili kuchagua viongozi wa kuleta maendeleo.