Share news tips with us here at Hivisasa

Kufuatia bunge la kaunti ya Mombasa kupitisha mswada wa kima cha shilingi million 9.9 siku ya Jumanne, wenyeji wamelitaka bunge hilo kupunguza mishahara yao na kutumia pesa wanazotengewa kufanyia maendeleo badala ya kuendelea kutumia hela kiholela ilhali kuna miradi mingi ya kaunti bado inahitaji kuangaziwa zaidi.

Akiongea kwa niaba ya wakazi siku ya Jumatano, Abubakar Mwinyi ambaye anapania kugombea mojawapo ya kiti cha uwakilishi wadi katika kaunti hiyo alisema kuwa sharti viongozi wa kisiasa kuangalia ni kipi kinahitaji kupewa nafasi kwanza na kuzingatia matakwa ya wakazi kwanza.

Alishangaa ni vipi kaunti hiyo ambayo ina masaibu chungu nzima inaweza kuzingatia hela za mishahara huku miradi mingi kama ya maji na miundomsingi bado ikipewa nafasi finyu, na kuwataka wakazi kuendelea kuwatia mkazo viongozi wao.

“Viongozi wa kaunti yetu wamekuwa na mbinu za kula hela tu kila mara, tunachosikia ni kuhusu kuongezewa mishahara na ni nadra kusikia masuala ya maendeleo, au miradi ambayo inawalenga wakazi katika kaunti,” alilamama kiongozi huyo.

Itakumbukwa kuwa wenyeji wamekuwa wakilalamikia matumizi mabaya ya hela na viongozi pamoja na waajiriwa katika ofisi na idara mbali mbali za kaunti na kuomba mtindo huo kukoma, lakini hata hivyo gavana wa kaunti ya Mombasa amewahakikishia wakazi kwa mara si moja kuwa atahakikisha kuwa miradi aliyowahidi wakati wa kampeni zake atatimiza kabla ya muhula wake.