Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baada ya gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho kuwataka wakazi ambao walidhulumiwa na maafisa wa polisi kuenda kortina, baadhi ya wakazi kutoka mitaa mbali mbali wamemwomba gavana huyo kuwapa wakazi ambao wataenda kortini msaada wa kupata mawakili ambao watawasaidia kuendeleza kesi kama hizo.

Wakazi hao walisema kuwa baadhi ya wakazi huenda wana nia ya kuenda kortini lakini hawana uwezo wa pesa kugharimia kesi, au baadhi ya wengine huenda wengine wakashikwa na hofu ya kuchukua kesi mahakamani.

Akiongea siku ya Jumapili kwa niaba ya wakazi wa mtaa wa Majengo ambao umeathiriwa mno na visa vya uhalifu na madai ya vijana kudhulumiwa na maafisa wa polisi, Uzinah Ramah alisema kuwa viongozi wa siasa sharti waonyesha nia na ari ya kuwafaa wakazi kupigania haki zao.

Uzina alisema kuwa mara nyingi, viongozi wa siasa wamekuwa wakisema mambo lakini hawatekelezi, na wakazi wanapotaka msaada kutoka kwao wanapotea na kuwaacha kuhangaika na uzito wa kesi za watoto ambao wamekuwa wakishikwa na maafisa wa polisi ambao wanadai kuwa huwadhulumu vijana hao na hata baadhi ya wana wa jamaa husika.

“Mara nyingi hawa wanasiasa watasema kitu kwa sababu ya kutaka kuwafurahisha wananchi na kutaka kupata kura, lakini naamini kuwa gavana wetu hatakuwa kama wanasiasa wengine, na namsihi kuonyesha vitendo na kuwapa vijana au mkazi yeyote ambaye amedhulumiwa bila kuwa na ushahidi wa kumhusisha na vitendo vya ugaidi,” alisema Uzinah.