Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baada ya lori moja lililobeba shehena kurudi nyuma na karibu kuwajeruhi watu waliokuwa wakiingia feri, sasa wakazi wa eneo la Likoni na baadhi ya wateja wa kivuko hicho wameitaka wizara ya barabara kuweka vizuizi sogevu pamoja na matuta ambayo yatazuia malori na magari mengine yenye uzani mkubwa kurudi nyuma yanapotoka kwenye feri.

Wakazi hao wamelalamikia ongezek0 la visa vya magari, hasa malori makubwa ya kubeba mizigo kutoka kwenye bandari ya Mombasa, kuwa na mazoea ya kuanguka ama kurudi nyuma, ambapo mara nyingi husababisha ajali kwa kuwagonga umma na magari ambayo huwa yanatoka kwenye feri.

Kwenye mahojiano na Ramadhan Mwambi siku ya Jumamosi, ambaye aliongea kwa niaba ya watumiaji wa feri hao, imekuwa ni mazoea ya malori kukwama yanapotoka kwenye feri, na hali hiyo imekuwa ikisababisha msongamano wa magari pamoja na watu kwa sababu magari yanapokwama hayatolewi mahali hapo kwa haraka.

Mwambi alishtumu usimamizi wa shirika la feri kwa kutojali, akitoa mfano wa lori lililokwama juzi na nusura kusababisha maafa na kuomba shirika hilo kuwa na namna mbadala za kuyashughukia masuala ya dharura na kuwa na magari ambayo yatarahisisha kazi ya kuyaondoa magari kwenye kivuko hicho yanapokumbwa na hitilafu ili kulainisha na kuimarisha huduma zao kwa wateja.