Wakazi pamoja na watumizi wa mara kwa mara wa kivuko cha Likoni wanapendekeza kwa shirika la feri nchini KFS kununua mashua na motaboti za kutumiwa na makundi maalum kama wanafunzi, wagonjwa pamoja na makundi mengine spesheli kila mara kunapozuka dharura.
Wakazi hao wamesema kuwa makundi mengi, hasa wagonjwa na wanafunzi wamekuwa katika hatari kubwa mara nyingi kunapotokea ukosefu wa feri za kutosha, hasa wakati feri hizo zianaharibika, hali ambayo huwafanya wanafunzi wengi kuchelewa kufika shuleni kwa wakati ufaao na wagonjwa kupoteza maisha au hali zao kuathirika zaidi.
Wakazi hao, wakiongozwa na mzee Ramadhan Mwanzi, siku ya Jumapili walisema kuwa imekuwa mtindo katika kivuko hicho kutowajali wanafunzi na wagonjwa kwani mara nyingi makundi hayo huwekwa pote moja na wengine, bila kuzingatiwa kwamba hali kama ya ugonjwa haitangojea na husababisha hata watu wengi kupoteza maisha wanapokuwa wakingoja feri hizo.
Mzee Ramadhan alisema kuwa ni jambo la kustajabisha sana kuwa shirika kubwa kama hilo halina mitambo mbadala ya kuvusha watu kama zile boti ndogo za kutumia mitambo ya injini, na kulitaka shirika hilo, kupitia usimamizi wake kuamka na kuishi na kuenda na wakati badala ya kukaa katika miaka ya sabini, nyakati ambako kila kitu kilitegea wanasiasa na wenye pesa kutoa huduma za kuridhisha.
Wakazi hao waliongeza sauti yao kwa serikali kuwa sharti mkurugenzi mkuu wa shirika hilo aondolewe ndio uchunguzi ufanywe kuhusiana na madai ya ufisadi ambayo yamezuka kuhusiana na jinsi shirika hilo linatekeleza shughuli zake.