Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana wawili wanaendelea kuuguza majeraha mabaya katika hospitali moja mjini Mombasa baada ya pikipiki waliyokuwa wameabiri kugongana ana kwa ana na nyingine iliyokuwa inaendeshwa kwa kasi mno katika kaunti ndogo ya Likoni.

Wawili hao walipata majeraha ya miguu na mikono baada ya kugongwa na pikipiki yao kubingiria mara kadhaa.

Wasamaria wema walioshuhudia ajali hiyo waliwashughulikia mara moja kwa kuwakimbiza hospitali ili kupata huduma za matibabu kwa haraka kwani walikuwa wanavuja damu nyingi.

Kijana huyo mwingine alikamatwa mara moja alipojaribu kukimbia eneo la tukio, na inasemekena kijana huyo vile vile alikuwa ameonja kinywaji ndiposa akakosa mwelekeo barabarani na kuwasababishia wenzake majeraha.

Kijana huyo alinusuriwa kutoka kwa umati uliokuwa na hasira na kupelekwa katika kituo cha polisi.

Wakazi wa kaunti hiyo hata hivyo wameitaka serikali ya kaunti kutoa mafunzo ya kina kwa waendesha pikipiki wote na kuhakikisha kuwa wana vyeti sahihi vya kuhudumu ili kupunguza ajali za kila mara.