Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wakazi kutoka eneo la Shika Adabu wamewasuta vikali wanasiasa kwa kutumia nafasi ya kujadili masuala ya maendeleo kupiga siasa, na kutaja malumbano kati ya Seneta wa Nairobi Mike Mbuvi na Gavana Ali Joho yaliyoshuhudiwa siku ya Jumamosi. 

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumamosi muda mchache baada ya malumbano ya viongozi hao wawili, mzee wa mtaa Nelson Mwakio alisema kuwa wanasiasa wanaleta aibu mbele ya hadhara ya rais, na kushangazwa na jinsi viongozi hao wawili walivyojivunia mbele ya umati ambao dhamira yao kuu ilikuwa ya kupokezwa hati za ardhi katika eneo hilo la Shika Adbu huko Likoni.

Mzee Mwakio aliwataka wanasiasa kujiepusha na siasa za kubomoa ukuaji wa uchumi na kujihusisha na mijadala ya kutafuta suluhu la kuweka masuala tata kama ya ardhi ambayo yamewakumba wakazi wa eneo la Pwani kwa muda mrefu badala ya kugawanya wakenya kwa misingi ya vyama na kikabila killa mara kunapotokea ziara ya kiongozi wa taifa katika maeneo mbalimbali humu nchini.

“Huwa ni aibu kubwa kila mara kuwaona wanasiasa ambao ndio viongozi wa kaunti zetu kuendelea kutoa matusi mbele ya raia wanaowaongoza kitu ambacho mara nyingi utia mbegu mbaya kwa vijana wetu ambao huwaangalia viongozi hawa kama mfano mwema kwao, na viongozi hawa wanachangia nchi kulea vijana ambao hawataheshimu sheria na ustarabu wa kijamii,” aliteta Mwakio.