Kulizuka kizazaa katika ukumbi wa CDF katika eneo la Likono mjini Mombasa siku ya Jumanne baada ya wakazi waliokuwa wakisubiri kukabidhiwa hati miliki katika shamba linalozozaniwa la Waitiki kuarifiwa kuwa watalazimikia kulipa shilingi elfu 182,000 ili kuweza kumiliki ardhi watakayogawiwa.
Kwa mujibu wa mshiriki wa mradi huo Joseph Kanyiri, wakazi hao watalipa kodi hiyo kwa muda wa miaka mitatu, ambapo baadaye wataruhusiwa kutwaa umiliki wa ardhi hizo.
Hali hiyo iliibua hisia kali baina ya maskwota na hata viongozi wa kisiasa waliotaja hatua hiyo kama unyanyasi kwa wakazi wasiojiweza kiuchumi.
Akizungumza katika eneo la tukio, mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko alitaka serikali kuigharamia ada hiyo.
‘’Ingekuwa vyema kama serikali ingelishughulikia suala hili kama ilivyowafanywa wakimbizi wa ndani kwa ndani. Hizo pesa ni nyingi kwa wananchi wa kawaida, afadhali walipishwe ada ya usoroveya,’’ alisema Mboko.
Haya yanajiri huku serikali ya Kaunti ya Mombasa kupitia waziri wa Anthony Njaramba ikidai kutohusishwa katika uamuzi wa kuwataka wakazi walipie ardhi hiyo.