Huku zoezi la usajili wa wapiga kura likiingia siku yake ya pili kote nchini, wakazi wa kaunti ya Mombasa wameshauriwa kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura ili kujihusisha kikamilifu katika kuwachagua viongozi wanaowaenzi.
Naibu mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya wanawake nchini Bi Sureya Hersi amesema kuwa iwapo wakazi wa kaunti ya Mombasa wana malengo ya kubadili uongozi wa taifa hili na hususan kaunti ya Mombasa, basi ni lazima kujisajili kama wapiga kura.
Sureya alieleza kuwa kaunti ya Mombasa imebainika kuwa na zaidi ya wakazi elfu 200 ambao bado hawajachukua vitambulisho vya kitaifa wala kadi za kura, hatua ambayo ameitaja kama changamoto kubwa katika maswala ya kuwachagua viongozi waadilifu.
"Tumebaini kuwa zaidi wa wakazi elfu 200 hawana vitambulisho vya kitaifa wala kadi za kura, hivyo basi tunawaomba wakazi wetu kujitokeza kwa wingi na kusajiliwa katika afisi za usajili wa watu ili wapate vitambulisho vya kitaifa na kujisajili kama wapiga kura,” alisema Sureya mjini Mombasa wakati wa mkutano wa hamasa siku ya Jumatatu.
Aidha, aliwataka maafisa wa tume ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini kuhakikisha kuwa wanazuru hadi mashinani na kuwahamasisha wakazi.
Kauli ya kiongozi huyo imeambatana na shinikizo za viongozi mbalimbali wa kisiasa wanaowashauri wafuasi wao kujisajili kwa wingi ili kuwabandua mamlakani viongozi walioshindwa kuwajibikia majukumu yao.