Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku zoezi la usajili wa wapiga kura liking’oa nanga kote nchini, makamishna wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC wamewashauri Wakenya kujitokeza na kujisajili kama wapiga kura.

Msimamizi wa Tume ya IEBC kanda ya Pwani kusini Gogo Nguma alisema kuwa usajili huo unalenga kuwasajili wakazi ambao bado hawajasajiliwa kama wapiga kura na wale waliyopoteza kadi zao za kura ama wanania ya kuhamia maeneo mengine ya kupiga kura.

Akiongea na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Nguma alisema kuwa tayari maafisa wa tume hiyo wametumwa katika kila wadi pamoja na mashini za usajili wa wapiga kura ili kufanikisha zoezi hilo bila pingamizi.

"Tumejiandaa vyema kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanyika vyema kwa sababu tumetuma maafisa wetu mashinani kufanya shughuli hiyo pamoja na vifaa maalum vya kusajili wapiga kura. Hivyo basi, tunawaomba wakazi kujitokeza kwa wingi,” alisema Nguma. 

Wakati uo huo, wananchi waliojitokeza kusajiliwa kama wapiga kura wamepongeza jinsi zoezi hilo lilivyokuwa likiendelea na kuwaomba wakazi kujitokeza ili kujisajili na kuwachagua viongozi waadilifu watakaoleta maendeleo.

“Tumefurahia kwa kuwa zoezi hili linaendeshwa vyema na maafisa hawa wa IEBC. Tunaomba wakazi ambao hawajajitokeza wafanye hivyo ili wajisajili,” alisema mmoja wa wakazi hao.

Zoezi hilo la usajili wa wapiga kura limepangwa kuendelea kwa kipindi cha mwezi mmoja huku tume hiyo ikilenga kuwasajili wapiga kura wengi zaidi.